Wednesday, 3 August 2016

There was an error in this gadget

WAZIRI MKUU AYAKATAA MADAWATI YALIYOTOLEWA NA TFS,

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekataa kupokea msaada wa madawati uliotolewa na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) baada ya kubaini yametengenezwa chini ya kiwango.

“Ofisa Elimu njoo kagua haya madawati yaliyo mazuri nitayapokea na yaliyobaki yarudishwe karakana yakatengenezwe upya huu si wakati wa kupokea vitu vibovu,“ amesema.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumanne, Agosti 02, 2016) wakati alipowasili katika kiwanja cha Mabau, Mtibwa kwa ajili ya kuzungumza na wananchi ambapo alikabidhiwa madawati hayo na Meneja wa TFS….

Alisema anatambua dhamira ya TFS ya kuunga mkono jitihada za Serikali za kumaliza tatizo la upungufu wa madawati lakini hawezi kupokea kupokea madawati yaliyotengenezwa chini ya kiwango.

Baada ya Ofisa Elimu (Msingi) wa Wilaya ya Mvomero, Michael Ligola kukagua madawati 102 yaliyoletwa uwanjani hapo madawati 84 yalibainika kuwa ni mabovu na 14 tu ndiyo yalikuwa mazima.

Waziri Mkuu alisema hawezi kupokea madawati hayo yaliyotolewa na Meneja wa Msitu wa Mtibwa, Hamza Kateti na kuuagiza uongozi wa wilaya ufuatilie suala hilo kwa kuwa walitakiwa kuyakagua kabla ya yeye kukabidhiwa.

Katika hatua nyingine aliwasisitiza wazazi na walezi wa wilaya hiyo kuhakikisha wanawapeleka watoto wao shule na atakayeshindwa atachukuliwa hatua kali za kisheria.

“Serikali imewapunguzia mzigo kwa kuwaondolea michango na ada hivyo tumieni fursa hiyo kwa kuwapeleka shule watoto wote waliofikia umri wa kwenda shule na wasimamie masomo yao,” alisema.

Awali mbunge wa jimbo la Mvomero, Saddiq Murad alisema miongoni mwa changamoto kubwa inayoikabili wilaya hiyo ni pamoja na wafugaji kuingiza mifugo katika mashamba hivyo amemuomba Waziri Mkuu kuingilia kati suala hilo.

Akizungumzia namna Serikali ilivyojipanga kutatua changamoto ya migogoro baina ya wafugaji na wakulima Waziri Mkuu alisema wafugaji wenye mifugo mingi watahamishiwa katika vitalu vinavyomilikiwa na ranchi za Taifa na wenye mifugo michache watatengewa maeneo katika vijiji.

KAMISHNA MSTAAFU WA MAGEREZA MAREHEMU EGNO KAMILIUS KOMBA.


Marehemu Kamishna Mstaafu wa Magereza. EGNO KAMILIUS KOMBA alizaliwa tarehe 20 Oktoba, 1947 katika Kijiji cha Mtungu - Kindimba Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma.

 Mwaka 1956 alijiunga na Elimu ya Msingi katika Shule ya Msingi Kindimba na kuhitimu elimu hiyo mwaka1959. 

Alijiunga na Shule ya Kati (Middle School) ya Litembo mwaka 1960 na kuhitimu mwaka 1963. Alijiunga na Shule ya Sekondari ya Kigonsera mwaka 1964 na kuhitimu Kidato cha Nne mwaka 1967. Mwaka 1968 alijiunga na Shule ya Sekondari Karimjee iliyopo Mkoani Tanga na kuhitimu mwaka 1968.

Marehemu aliajiriwa na Jeshi la Magereza tarehe 02 Agosti, 1972 na kupelekwa kuhudhuria mafunzo ya awali ya Uaskari katika Chuo cha Usalama – Moshi. Marehemu alihitimu mafunzo hayo tarehe 30 Aprili, 1973 na kupangiwa kufanya kazi Gereza Malya, Mkoa wa Shinyanga.

Mwaka 1975 akiwa mwajiriwa wa Jeshi la Magereza, Kamishna mstaafu wa Magereza, Marehemu EGNO KAMILIUS KOMBA alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es salaam kwa ajili ya masomo ya Shahada ya Kwanza katika Uchumi na kuhitimu mwaka 1978.

Marehemu akiwa Jeshini alitunukiwa vyeo mbalimbali kama ifuatavyo:-
Afisa Magereza Daraja la III (PO III)​– ​30/04/1973 – 31/09/1973

Afisa Magereza Daraja la I (PO I)​​- ​01/09/1973 - 31/06/1976
Afisa Magereza Mkuu (PPO)​-​01/07/1976 - 30/11/1978
Mrakibu Msaidizi wa Magereza (ASP)​- ​01/12/1978 - 31/09/1980
Mrakibu Mwandamizi wa Magereza (SSP)​ - ​01/10/1980 -31/12/1996
Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP) ​- ​01/07/1984 -19/09/1989
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza (SACP)-20/09/1989-30/6/1996
Kamishna wa Magereza (CP) ​- ​01/07/1996 - 30/06/2007 (Alipostaafu kwa umri Mkubwa).

Marehemu alifanya kazi katika vituo vifuatavyo vya Magereza:-
Gereza Malya – Shinyanga ​- Tarehe 01/05/1973 - 12/05/1974
Makao Makuu ya Magereza ​- Tarehe 13/05/1974 – 30/06/2007

Katika utumishi wake Jeshini Marehemu pia alitunukiwa nishani mbalimbali kama ifuatavyo:-
•Nishani ya Mstari wa Nyuma ya Vita vya Kagera,
•Nishani ya Utumishi Mrefu Tanzania na,
•Nishani ya Utumishi Uliotukuka.
Katika utendaji wake wa kazi, Marehemu alikuwa na uwezo mkubwa wa kujifunza, kutawala na kuyamudu majukumu yake ya kazi ipasavyo. Viongozi na watumishi wa Jeshi la Magereza tunamlilia mno kwa Utumishi wake uliotukuka na hazina kubwa ya utendaji aliyoondoka nayo kwani hata baada ya kustaafu katika Jeshi la Magereza bado alikuwa akitoa ushauri katika mambo mbalimbali ya Uendeshaji wa Jeshi la Magereza.

Kamishna Mstaafu wa Magereza EGNO KAMILIUS KOMBA alikuwa anasumbuliwa na Ugonjwa wa Moyo hadi umauti ulipomkuta mchana ya tarehe 31 Julai, 2016 nyumbani kwake Mvuti, Chanika Jijini Dar es Salaam. Mwili wa Marehemu unatarajiwa kuzikwa kesho Agosti 3, 2016 Shambani kwake Mvuti, Jijini Dar es Salaam.

MWENYEZI MUNGU AIWEKE PEMA PEPONI ROHO YA MAREHEMU EGNO KAMILIUS KOMBA, AMEN.

YANGA KUCHEZA MECHI YA KIRAFIKI NA MTIBWA.

Katibu Mkuu wa Yanga Baraka Deusdedit.

Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii.
TIMU ya Yanga inatarajia kucheza mchezo wa kirafiki na Mtibwa Sugar Agosti 08 ikiwa ni maandalizi ya kuendelea mchezo wao wa kimataifa dhidi ya Mo bejaia unaotarajiwa kupigwa Agosti 13 Jijini Dar es salaam.

Akizungumza na Mtandao huu, Katibu Mkuu wa Yanga Baraka Deusdedit amesema kuwa mechi hiyo itatumika kwa ajili ya kukiangalia kikosi kabla ya kuelekea mchezo wao wa kimataifa wa kombe la Shirikisho ambapo wana nafasi ndogo sana ya kufuzu ila bado hawajakata tama kwani kama wakifanikiwa kushinda michezo ilioyobaki pia inakuwa ni moja ya nafasi nzuri watakayokuwa nayo katika kundi A.

Deusdedit amesema kuwa, kwa sasa wachezaji wanaendelea na mazoezi katika viwanja vya Gymkhana na wachezaji wote wako vizuri isipokuwa Geofrey Mwashiuya ambaye bado ana P.O.P ila wengine wameanza mazoezi ua pamoja.

Mbali na hilo pia katika siku hiyo hiyo, Uongozi wa Yanga umetangaza kuitisha mkutano mkuu wa wanachama watakaojadili masuala ya ndani ya klabu yao pamoja na maendeleo kwa ujumla kuelekea ligi kuu na nini cha kufanya ambapo unatarajiwa kuanza majira ya saa 3 asubuhi katika ukumbi wa Diamond Jubilee na baadae watajumuika pamoja Uwanja wa Taifa kushuhudia mtanange huo wa kirafiki.

No comments:

Post a Comment