Thursday, 22 September 2016

MECHI ATAKAZO KOSA MESSI BAADA YA MUUMIA

Usiku wa Septemba 21 Ligi Kuu Hispania iliendelea kama kawaida kwa michezo kadhaa kupigwa, lakini moja kati ya michezo iliyochezwa ni pamoja na mchezo kati ya FC Barcelona dhidi ya Atletico Madrid uliomalizika kwa sare ya goli 1-1.
FC Barcelona ambao walikuwa katika uwanja wao wa nyumbani walipata pigo katika mchezo huo ambapo mchezaji wao tegemeo Lionel Messi aliumia mguu wake wa kulia dakika ya 51 na kutolewa nje na nafasi yake kuchuliwa na Arda Turan.
Leo Septemba 22 2016 taarifa zimetoka Lionel Messi atakaa nje ya uwanja kwa wiki tatu na atakosa michezo sita dhidi ya Sporting GijonGladbachCelta VigoDeportivo la Coruna na anatazamiwa kuwa fiti katika mchezo wa UEFA Champions League dhidi yaMan City October 19 2016.

UTEMI WA CHIEF FUNDIKILA

Mtemi Fundikira III ( Abdallah Said)

Mtemi Fundikira(III)Abdallah Said.(1957-1962).1957-2007

Hili ni kaburi la Mtemi Fundikira III, katika Ikulu ya Itetemya.

Huyu alikuwa Mtemi wa 19  wa Unyanyembe. Utawala wake ulidumu kwa miaka 5 kuanzia mwaka 1957 mpaka 1962. Baada ya Tanganyika kupata uhuru 1961 ndipo Mwalimu Nyerere alipofuta utemi wa dola rasmi mwaka 1962. Mtemi huyu ana historia kubwa sana katika nchi ya Tanganyika pamoja na kuwa haipewi nafasi katika vitabu vya historia na kwingineko. Baada ya hapo alibaki kuwa Mtemi wa jadi tu na asiye na nguvu yeyote ya kuendesha serikali mpaka alipofariki usingizini nyumbani kwake Mwanza Road, Tabora mnamo tarehe 8/8/2007.
Historia zaidi kuhushu Mtemi Fundikira III zitafuata... 
Hapa akiwa nje ya Ikulu ya Itetemia 1957.
Ikulu yake iliyopo Itetemia

Mtemi Fundikira III akitawalishwa 1957

Friday, April 15, 2011

Mtemi Fundikira II (Nassor Said) kimala masasi!

Mtemi Fundikira II( Nassor Said)

Dirisha la chumba alichojipigia risasi Mtemi Fundikira III 1957.
Alitawala kuanzia mwaka 1948 mpaka 1957, utawala wake ulidumu kwa miaka 9. Mtemi huyu alipotawala aliweka mikakati ya kukomesha wizi wa mifugo, aliwatangazia wezi wote wajisalimishe kabla hawajatafutwa na kukamatwa, na kweli wezi wote wa mifugo walijisalimisha na wizi wa mifugo hasa ng'ombe ukaisha kabisa katika nchi ya Unyanyembe na jambo hili lilipelekea akatunukiwa medali ya heshima iitwayo ORDER OF THE BRITISH EMPIRE (OBE) na Malkia Elizabeth II katika Ikulu yake Buckingham Palace mjini London. Hii ni heshima kubwa sana ambayo si watanzania wengi wamewahi tunukiwa medali hiyo. Baadae mwaka 1957 ulitokea ubadhirifu wa pesa za serikali katika nchi yake Unyanyembe na ilikuwa dhahiri yeye ndiye kazila, askari wa kikoloni (Waingereza) walipotaka kumkamata akajifungia chumbani mwake na kujipiga risasi na kufa.
Mtemi Fundikira II (Nassor Said) Order of the British Empire.

Mtemi Mkasiwa ( Ilagila)

Mtemi Mkasiwa alitawala kuanzia mwaka 1932 mpaka 1948 na utawala wake kudumu miaka 16. Huyu hakutaka kutawala ila alilazimishwa na ndio sababu ya kuitwa Mkasiwa. Pia huyu alikuwa ni mtu wa aina yake, kwani yeye alikuwa binti ya Mtemi kisha akaolewa na Mtemi Mkwawa na baadae akawa Mtemi wa Unyanyembe. 

Mtemi Kiyungi Mwana Isike

Huyu alikuwa mtoto wa Mtemi Isike mwana Kiyungi alitawala kuanzia mwaka 1928 mpaka 1932.

Mtemi Saidi Fundikira (Sultan Said)

Hili ndilo kaburi la  Mtemi Swetu(Said) Fundikira alizikwa hapo mwaka 1961.
Mtemi Saidi Fundikira (Sultan Said) huyu alikuwa Mtemi maarufu sana katika nchi ya Tanganyika, alitawala kuanzia mwaka 1917 mpaka 1927. Alifanikiwa kuwashawishi watemi wengine  wa kanda ya magharibi kuchanga pesa, mifugo na mali nyingine ili

Mtemi Said (sultan said) Fundikira 1956
Sultan Said Fundikira na Mw Nyerere 1956

Mzee Ramadhani said Fundikira

kupata pesa za kujenga shule mbili za Tabora Boys na Tabora Girls. Na yeye akatoa ardhi ya kujenga shule hizo kwa kuwa eneo hilo lilikuwa chini ya himaya ya Ikulu ya Unyanyembe. Vile vile Mtemi Said alikuwa mkarimu mno kiasi kwamba mtu akiunguliwa na nyumba yeye alimjengea nyumba mpya na kumpa chakula cha kumtosha kwa mwaka mzima. Na kila mwisho wa mwezi alipokuwa akitoka Bomani kuchukua mshahara wake ulikuwa ni shilingi 4000, ambazo hata Gavana wa Kiingereza Bw Donald Cameron alipata kiasi hicho pia. Watu wenye shida walijpanga katika barabara ya Luhanzali wakimtolea shida zao naye aliwasaidia kwa kuwapa pesa za mshahara wake na hata alipofika Ikulu Itetemia alijikuta kuwa ameishiwa pesa zote.  

Yeye aliondolewa madarakani na wakoloni wa kiingereza baada ya kuwa hapeleki serikalini kodi aliyotoza wananchi, inasadikika alitumia pesa hizo kusaidia masikini. Hivyo kwa heshima na upendo aliyokuwa nao kwa wananchi wake wakoloni wa Kiingereza walilazimika wasimfunge jela ila walimuondosha Itetemia na kiti chake akakitwaa Mtemi Kiyungi II huyu alikuwa mtoto wa Mtemi Isike Mwana Kiyungi. 

Sultan Said alijaaliwa kupata watoto 57 ambao miongoni mwao ndio hawa kina marehemuChief Abdallah Fundikira, Ramadhani Mlawila (Baba yangu), Kagori biti Said (Mama yake Samuel Sitta) na wengi wengine.Na mpaka sasa katika watoto hao 57 wamebaki wanawake watatu Kagori na Ndisha na mwanamume mmoja Ramadhani Mlawila (87)aliyepata kuwa waziri mkuu katika ofisi ya Mtemi Fundikira III pia aliwahi kukaimu Utemi wakati Mtemi Abdallah (Fundikira III) alipoingia serikalini.

Nyumba hii ilitumiwa na waziri mkuu Mlawila 1957-64

Ninavyofikiri mimi Sultan Said ndiye aliyeuingiza ukoo huu wa Fundikira katika dini ya ki Islam, kwa kuwa yeye alisomea Zanzibar ambako dini hiyo ilishasambaa huko. Bila shaka aliporudi bara ndipo akaja na dini hiyo ambayo mpaka sasa ndiyo imekua dini ya Ukoo huu. Na hakuna ushahidi kama ukoo huu uliwahi kuwa waumini wa dini yeyote kabla miaka ya 1900. Hivyo basi inaelekea ukoo huu uliabudu mizimu kama ilivyo desturi ya wa Afrika.
Sultan Said aliishi katika nyumba hii baada ya kuruhusiwa kurudi Itetemia

Mtemi Kalunde Mwana Gumadi

Hili ndilo kaburi la Mtemi Kalunde Mwana Gumadi alitawala 1896-1917


Alitawala baada ya Mtemi Nyamso kufariki mwaka 1896, naye alitawala kuanzia mwaka huo huo mpaka mwaka 1917. Mtemi huyu alikuwa mwadilifu sana na alipenda kusaidia watu kutatua matatizo yao, alikuwa akiamka saa 12 asubuhi na kupita kwenye maofisi kukagua kazi mbali mbali na pia kuona kama maafisa wake wamekwenda maofisini mwao kusikiliza shida za wananchi. Na inapofika mchana chakula kinapokuwa tayari alikuwa akipiga kengele ili mtu yeyote aliyepita hapo aende akale, kwa kifupi alikuwa mtu mkarimu sana. Ilipofika mwaka 1917 alifariki.

JUA HISTORIAKWAUFUPI YA WACHAGA

WACHAGA ni kabila la kibantu linalopatikana Kaskazini mwa Tanzania katika mkoa wa Kilimanjaro.

Wachaga wanajishughulisha na kilimo cha viazi, ndizi na mtama. Zao la kahawa lilianzishwa na wakoloni karne ya 19 na kuendelezwa hadi leo kama zao la biashara. Pia wachagga hujihusisha na ufugaji wa ng'ombe, mbuzi na kondoo ili kupata samadi ya kurutubisha mashamba, nyama, maziwa.

Miaka ya nyuma ufugaji wa mbuzi au kondoo ulikuwa wa lazima ili kupata wanyama wa kutambika. Ilikuwa ni mwiko kutambika kwa kutumia mnyama wa kununua au kutoka nyumba nyingine. Kutokana na uhaba wa ardhi katika makao yao ya asili, Wachaga wametawanyika sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi wakijishughulisha na kazi mbalimbali ili kupambana na umasikini.

Ingawa baadhi ya hadithi za kale zinaeleza kuwa Wachaga walikuwepo eneo la Kilimanjaro na dua zao ndizo zilizorefusha mlima Kilimanjaro ili waweze kuwa karibu na Mungu, utafiti unaonesha kuwa Wachaga ni wahamiaji waliofika Kilimanjaro miaka 600 kabla ya ujio wa Kristo. Hivi sasa ni zaidi ya miaka 2000 baada ya Kristo.

Tafiti kuhusu makabila zinasema endapo Wachaga wataamua kutafuta asili yao kwa kuzingatia kizazi cha kale ni lazima wabishe hodi kwenye jamii za makabila mbalimbali hasa kwa Wakamba, Wamaasai na Wataita nchini Kenya, pia kwa Wapare, Wasambaa nchini Tanzania.

Tofauti na makabila mengine ambayo asili yao inatokana na kizazi kimoja, Wachaga wanaweza kujua asili ya kizazi chao kwa kufuatilia historia ya ukoo au historia ya makundi kulingana na eneo. Historia ya kale inasema kuwa jamii ya wachaga inatokana na watu wa makabila mbalimbali ambao walihamia kwenye mteremko wa mlima Kilimanjaro baada ya kukimbia vita na wengine kukimbia baa la njaa.

Pia wapo waliohamia eneo hilo baada ya kuvutiwa na ardhi yenye rutuba na hali nzuri ya hewa na inasemekana kuwa wahamiaji hao waliwazidi nguvu wenyeji wa eneo hilo ambao walijulikana kama Koningo au Konyingo. Baadhi ya wenyeji walihama ila inasemekana kuwa wengine walibaki na kujumuika na wahamiaji na baada ya kuishi pamoja kwa muda mrefu waliunda kabila jipya la wachaga.

Ingawa hakuna ushahidi wa kisayansi kuwa Wachaga walitokana na makabila mengine, simulizi za kale na mfumo wao wa maisha unadhihirisha kuwa hawatokani na kizazi kimoja wala wazee na viongozi wao hawajawahi kuwa na uhusiano wa karibu.

Ingawa watu hao huitwa wachaga wenyewe ni vigumu kujua nani hasa ni Mchaga kwa kuwa wenyeji hutambuana kwa kutumia lugha ya eneo husika kama vile Mrombo, Mmachame, Muuru, Mkibosho au Muanjo akimaanisha mchaga wa Marangu. Uongozi wa jamii ya Wachaga ulitumia mfumo wa machifu, maarufu kama Mangi.

Kila eneo lilikuwa na mangi wake, ila Mangi Sina wa Kibosho, Rindi wa Moshi na Marealle wa Marangu walipata umaarufu mkubwa, kutokana na jitihada zao za kutaka kuwa wafalme ili kutawala himaya nzima ya wachaga. Hata hivyo, jitihada hizo ziligonga mwamba kwa kuwa hakuna Mangi aliyekuwa tayari kutawaliwa na kiongozi kutoka kundi jingine.

Hali ya kujihami na kuogopana inachukuliwa kama kielelezo kuwa chimbuko la wachaga linatokana na jamii za makabila tofauti yenye historia tofauti.

Mfumo wa uongozi miongoni mwa wachaga umeathiri kizazi kipya kwa kuwa uzoefu unaonesha kuwa wachaga ni miongoni mwa jamii chache zinazopenda siasa za upinzani na hupenda kuchagua kiongozi kwa kupima uwezo wa mtu badala ya chama.

Kati ya mwaka 1750 na mwaka 1890 Wachaga walikuwa na vita vya mara kwa mara, ambapo kila Mangi alitaka kutwaa eneo la mwenzake ili kuongeza ukubwa wa ardhi na kuimarisha ngome yake kiuchumi.

Hadi Mwanzoni mwa Karne ya 19 , wachaga waligawanyika katika makundi 30 na kila kundi lilikuwa na Mangi wake na walijitegemea mithili ya nchi 30 katika kisiwa kidogo chenye udongo wenye rutuba, hali ya hewa safi na chemchemi za maji kila baada ya hatua chache.

Wachaga walikuwa na bendera yao na siku maalumu ya mapumziko, maarufu kama Siku ya Wachaga, ambapo watu walikutana kwa ajili ya kula na kucheza pamoja ili kuimarisha mshikamano upendo na mshikamano. Makundi hayo yalizungumza lugha tofauti na lahaja tofauti, kulingana na jiografia ya eneo husika.

Watu hao waliwindana kila mmoja akimnyooshea mwenzake kidole kwa uchokozi na tamaa ya kutwaa mali na ardhi ya kundi jingine. Vita vya wachaga viliimarika baada ya kuingia kwa Wamisionari, ambao walifika Kilimanjaro na kueneza dini ya Kikristo pamoja na kuanzisha zao la kahawa.

Hivyo, machifu waliweka silaha chini na kuelekeza nguvu zao kwenye kilimo cha kahawa. Wakoloni walifurahi hali ya utengano miongoni mwa Wachaga hivyo walitumia fursa hiyo kuwalaghai machifu ili waweze kupata ardhi kubwa na rasilimali nyingi. Kila chifu alijitahidi kuwakarimu wageni ili aweze kupata msaada wa kujiimarisha kiuchumi na kisiasa.

Kwa mujibu wa historia ya Wachaga, iliyoandikwa na Stanl Kathleem mwaka 1962, kabila hilo lilikuwa na viongozi wengi, ila wachache walipata umaarufu kutokana na aina ya uongozi wao.

Mwaka 1800 chifu aliyejulikana kama Mangi Horombo kutoka Mashariki mwa mlima Kilimanjaro, alikuwa na nguvu zaidi na aliweza kutwaa maeneo yaliyokuwa na wachaga wasiokuwa na nguvu kiuchumi wala kisiasa.

Hata hivyo baada ya kifo cha Horombo himaya yake iligawanyika na kuunda vikundi vidogo vinavyojitegemea. Wakati Muingereza wa kwanza, Johannes Rebmann, alipofika Kilimanjaro mwaka 1848 alikuta mangi wa Machame na Mangi wa Kilema wakiwa na nguvu kubwa kisiasa na kiuchumi, lakini alififia kutokana na sababu mbalimbali.

Kathleem anasema Mangi Oromba alikuwa kiongozi jasiri katika eneo la Mashariki mwa Mlima Kilimanjaro na aliogopwa na watu wake kwa kuwa alikuwa mtu mwenye msimamo. Kiongozi huyo aliishi eneo ambalo hivi sasa linafahamika kama wilaya ya Rombo. Alikuwa Mangi wa kwanza kuanzisha wazo la kujenga himaya ya Wachaga.

Alijenga ngome yake katika kijiji cha Keni na kuunja jeshi, ambalo lilivamia himaya za machifu wengine na kufanikiwa kuteka eneo la Vunjo hadi mto Nanga. Hata hivyo, baada ya kifo chake himaya yake iligawanyika na kurudi katika vikundi vidogo vidogo kwa kizingatia asili na chimbuko la kila kikundi.

Mangi Sina alikuwa jasiri kama Orombo na aliyongoza himaya ili- yokuwa Magharibi mwa mlima Kilimanjaro hadi mpakani kwenye mto Nanga. Alijenga ngome yake katika eneo la Kibosho, ila alitawala hadi eneo la Marangu na Uru. Mwaka 1870 alijenga mji wa kibiashara kati ya Waafrika na Waarabu, ambapo waarabu walimpa nguo na silaha kisha akatoa pembe za ndovu vitu vingine vya thamani.

Utawala wa Mangi Sina ulififia mwaka 1891 wakati waingereza walipoamua kumuongezea nguvu Mangi Rindi wa Moshi, kisha kumtumia kudidimiza utawala wa Mangi Sina. Mangi Rindi ambaye alijulikana kwa jina la Mandara, alikuwa kiongozi wa Moshi mwaka 1860. Alikuwa miongoni mwa viongozi waliokuwa na ndoto ya kutawala eneo lote la Kilimanjaro.

Ili kufanikisha mikakati yake aliungana na viongozi wa kabila la Arusha eneo la mlima Meru na waswahili kutoka Pwani, kisha kusaini mkataba wa Wajerumani kwa lengo la kuiweka Kilimanjaro chini ya Utawala wa kijerumani katika Ukanda wa Afrika Mashariki.

Mwaka 1891 alifanikiwa kuhifadhi ngome ya kijeshi ya Wajerumani kwa ajili ya kusambaratisha utawala wa Mangi Sina wa Kibosho. Uhusiano wa Mangi Rindi na Wajerumani, uliwezesha Moshi kuwa makao makuu ya mkoa wa Kilimanjaro hadi mwaka 1919 wakati makao ya mji huo yalipohamishiwa eneo la kudumu ulipo mji wa Moshi hivi sasa.

Mangi Marealle wa Marangu alisimikwa na Mangi Sina mwaka 1880 wakati eneo la Marangu lilipokuwa sehemu ya himaya ya Kibosho.

Mangi Marialle wa kwanza alikuwa kijana mwerevu na mwenye shauku ya kuwa kiongozi bora kuliko waliomtangulia Kwa kuwa Mangi Marealle hakuwa mtu wa kutumia mitutu, aliamua kujifunza lugha ya kigeni ili kuweza kuwasiliana moja kwa moja na viongozi wa Kiarabu na wakoloni wa Kiingereza na kuwaalika kuwekeza katika eneo la Marangu.

Pia, alijaribu kujenga urafiki na uongozi wa utawala wa Kijerumani na inadaiwa inadaiwa kuwa 1890 Mangi Marealle alifanikiwa kushawishi uongozi wa jeshi la Kijerumani, kuamini kuwa kuwa watu wa kibosho na Moshi walikuwa na njama ya kuangusha kutawala wa Kijerumani, jambo ambalo lilisababisha machifu wa Kibosho na Moshi kunyongwa na utawala wa Kijerumani.

Himaya ya Watu wa Machame ilijengwa na Mangi Abdiel Shangali, ambaye aliingia madarakani mwaka 1923 na kuongoza mfululizo hadi mwaka 1946 alipopandishwa cheo na kuwa chifu wa jimbo la Hai, kwa kujumuisha eneo la Machame na kibosho.

Mangi Shangali alitawala kipindi cha amani, hivyo alifanikiwa kubadilisha mfumo wa uongozi kutoka utawala wa kichifu wa kuridhishana hadi utawala wa mfumo wa kisasa kwa kuchagua viongozi kwa njia ya demokrasia.

Hata hivyo, wachaga hawakuacha kuzozana kuhusu uhaba wa ardhi na hali hiyo iliendelea hadi Tanganyika ilipopata uhuru na kufunja mfumo wa utawala kitemi na kuunda serikali ya umoja wa Kitaifa. Baada ya Uhuru wachaga waliendelea kukodoleana macho kila kundi likitamani ardhi ya kundi jingine.

Hata hivyo Rais Nyerere alifanikiwa kumaliza tatizo hilo kwa kuwahimiza wachagga watawanyike na kushika ardhi katika maeneo mengine katika ardhi ya Tanzania badala ya kung'an'gania ardhi ndogo katika mteremko wa mlima Kilimanjaro.

Hali hiyo iliwafanya Wachaga kuamua kuwekeza katika elimu ili kuwawezesha watoto wao kujenga uwezo wa kujitegemea na kwenda kutafuta maisha sehemu nyingine. Hali hiyo imewawesha wachagga kutawanyika sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi kujitafutia maisha kwa kushiriki katika nyanja mbalimbali hasa katika uongozi wa mashirika, ualimu na biashara.

Watafiti wa masuala la kisiasa wanasema mfumo wa maisha ya Wachaga, umesababisha watu wa kabila hilo kuwa washabiki wa siasa zenye upinzani kutokana na tabia yao ya kujihami kisiasa.

Ingawa viongozi kadhaa wa juu wa vyama vya upinzani wanatoka mkoa wa Kilimanjaro, inaelezwa kuwa ni vigumu viongozi hao kuunganisha vyama vyao na kuunda chama kimoja chenye nguvu, kutokana na ukweli kuwa hata Machifu wa zama za kale, walishindwa kuungana na kuchagua mtawala mmoja.

Kama ilivyo kwa Watanzania wengine, Wachaga wanapokuwa katika mikoa au nchi tofauti, husahau tofauti zao za nyumbani na kushirikiana kama ndugu wa mama mmoja. Hali hiyo imewezesha wachagga kuishi popote na kushirikiana na watu wa makabila mengine bila kusahau utamaduni wa kwenda kwao angalau mara moja kila mwaka.

Naamini umeelimika sasa!!

HISTORIA FUPI YA MTEMI MILAMBO

JINA la Milambo ni maarufu sana hapa Tanzania na katika eneo lote la ukanda wa Afrika Mashariki. Lakini ni watu wachache wanaoweza kueleza Milambo ni nani na alifanya nini hadi kustahili sifa kubwa kiasi hicho.

Kutokana na sifa hizo, hivi leo, kuna mtaa moja katika Jiji la Dar es Salaam uliopewa jina lake. Huko Tabora, Shule ya Sekondari na kambi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) vimepewa jina la Milambo. Kumbukumbu kama hizo zinaashiria kwamba Milambo alikuwa ni mtu maarufu.

Mtemi Milambo alizaliwa kwenye miaka ya 1840 katika tawala ndogo ya Ukune katika eneo la Unyamwezi, Mkoa wa Tabora Tanzania. Baba yake alikuwa mtemi Kasanda wa Uyowa katika wilaya ya sasa ya Urambo. Mama yake aliitwa Masele Nyakasi au Nyakashi wa uzawa wa Mtemi Kifumigulu mkimbu kutoka Ikungu aliyefika Usumbwa na kuanzisha tawala ndogo ya Ukune. Kifumigulu alikuwa ni mtoto wa Mapokela Kiumbe I mtemi wa Ikungu.

Kifumigulu na ndugu yake Magokola waliondoka Ikunga kwenda Usumbwa kuwinda tembo na kufanya biashara. Lakini baada ya kugundua kwamba wenyeji waliowakuta hawakuwa na nguvu, waliweza kuanzisha tawala mbili za Ukune na Uyogo.

Milambo mwenyewe alizaliwa Ukune kwani Nyakasi alipokuwa na mimba na kwa sababu alikuwa ni mimba ya kwanza alirudi kwa wazazi wake kwenda kujifungua.

Nyakasi alijifungua mtoto wa kiume aliyepewa jina la Mbula Mtelya.
Milambo alikulia Uyowa na baba yake mtemi Kasanda alipofariki, Milambo alirithi utawala wa Uyowa.

Kasanda alikuwa na Jeshi lake ambalo masimulizi yanaeleza kuwa aliliongoza kwa ushupavu mkubwa lakini kwa sababu Uyowa ilikuwa ni tawala ndogo yenye watu wapatao 4,000 wakati Milambo anatawazwa, hakuweza kuingia kwenye mapambano makubwa kama alivyofanya Milambo baadaye.

Kwa kutambua kikwazo hicho cha udogo wa tawala ya Uyowa aliyoirithi kutoka kwa baba yake, Milambo aliamua kuondokana na kikwazo hicho. Miaka miwili tu baada ya kuwa mtemi wa Uyowa, Milambo alivamia tawala ya jirani ya Ulyankulu na kuiunganisha na Uyowa na kuzitawala zote mbili kwa pamoja. Baadaye tawala hizo mbili zilikujajulikana kama Urambo jina ambalo linatumika hadi leo.

Milambo aliishi na kutawala katikati ya karne 19. Katika kipindi hicho mambo mengi yalikuwa yanatokea ulimwenguni ambayo yalianza kuligusa bara la Afrika ikiwemo Afrika Mashariki.

Unyamwenzi ni eneo kubwa lakini wananchi wake waligawanyika katika tawala nyingi ndogondogo zilizo huru na zisizo na mshikamano. Hali hiyo ilizifanya tawala hizo kuwa dhaifu kijeshi na katika ushindani kibiashara. Biashara kubwa ya wakati huo ilikuwa ni Pembe za tembo, watumwa na shaba.

Watemi wengi wa Kinyamwezi walipeleka misafara pwani kwenda kuuza pembe za tembo na kisha kununua, nguo, majembe, mahitaji ya kijeshi, shanga na vitu vingine vya wakati huo.

Katikati ya karne ya 19 wafanyabiashara wa Kiarabu waliingia Unyamwezi wakiongozwa na Musa Mzuri ambao walifanya makazi yao Unyanyambe, moja ya tawala muhimu ya Unyamwezi.

Baadaye alifika Muhammad bin Juma, baba yake Tippu Tipu. Muhammad Bin Juma alihalalisha ukazi wake Unyanyambe kwa kumuoa Kalunde, binti ya mtemi Fundikira wa Unyanyembe. Hapo ndipo ushindani wa kibiashara kati ya Waarabu na Wanyamwezi ulipojitokeza kwa nguvu zaidi.

Milambo hakupenda biashara yote idhibitiwe na waarabu na maliasili zichukuliwe bila ya wenyeji kufaidika nazo. Milambo ameelezwa na waliomwona kuwa alikuwa na urefu wa wastani, mwenye mwili imara na mwenye akili nyingi na alikuwa tayari kusikiliza ushauri lakini uamuzi alifanya yeye. Mara akisha kuamua, Milambo alitekeleza maamuzi bila kuchelewa.

Milambo alikuwa mkatili na hakuvumilia utovu wa nidhamu miongoni mwa wasaidizi wake na wananchi kwa ujumla wake.

Katika mazingira ya kukabiliana na ushindani, Milambo aligundua kuwa Uyowa na Ulyankulu peke yake zisingempa uwezo wa kupambana na wageni. Na kwa vile isingekuwa rahisi kuwaelimisha na kuwaunganisha Wanyamwezi kwa hiyari, alitumia nguvu za kijeshi.

Katika kipindi kifupi aliweza kuzivamia na kuziingiza chini ya himaya yake karibu tawala zote za Kinyamwezi isipokuwa Unyanyembe.

Wakati wa kilele cha mafanikio yake, Milambo alidhibiti eneo lote kuanzia Ziwa Victoria hadi bonde la Ziwa Rukwa.

Katika eneo lote hilo hakuna msafara uliopita bila kibali cha mtemi Milambo.

Katika mwaka 1871 Milambo alijitokeza kama mtawala asiye na mpinzani katika ukanda wote wa Afrika Mashariki kufuatia mapambano kati yake na Waarabu walioweka ngome yao Unyanyambe.

Jamii ya Waarabu na Unyanyembe wakisaidiwa na Mtemi Mkasiwa waliandaa jeshi kubwa kupambana na Milambo na kumaliza nguvu zake kabisa.

Lakini Kabla hatujaangalia kisa hiki ni vizuri kusimulia yaliyokuwa yanatokea Unyanyembe hadi kusababisha Mkasiwa (Mnyamwezi) kushirikiana na Waarabu kumwangamiza Milambo.

Tumeona hapo awali kwamba Waarabu wa kwanza wakiongozwa na Mussa Mzuri walifika Unyanyembe wakati mtemi Fundikira I akitawala.

Baadaye jamii ya kiarabu na wa fanyabiashara wa Kiswahili ilipanuka hadi kumfanya Sultan wa Zanzibar kumteua Said bin Salim kuwa liwali wa Unyanyembe.

Katika kipindi hicho waarabu waliweka fungamano na mtawala wa Unyanyembe kwa Muhammad bin Juma (Baba wa Tippu Tip) kumuoa binti wa Mtemi Fundikira I Kalunde.

Bila ya watawala wa Unyanyembe kujijua, kuteuliwa kwa liwali kumwakilisha Sultan wa Zanzibar na mwarabu kumuoa mtoto wa mtemi, kulianza kupunguza nguvu za watawala* wa Unyanyembe na hili lilijidhihirisha waziwazi baada ya kufa Mtemi Fundikira I mwaka 1858.

Baada ya Mtemi Fundikira I kufariki 1858 kulitokea msuguano nani arithi utemi wa Unyanyembe. Katika msuguano huo mshindani aliyeungwa mkono na jamii ya Waarabu alifanikiwa. Tayari Waarabu walisha anza kuwa na nguvu dhidi ya watawala wa Unyanyembe. Mtemi Msabila au Mnywa Sele kama alivyopenda kujiita yeye mwenyewe,* alimrithi Fundikira 1 kwa msaada wa Waarabu.

Mtemi Mnywa Sele alikuwa mkakamavu, mpenda biashara na mzalendo kweli kweli wa Unyanyembe. Haukupita muda Mnywa Sele akagombana na washirika wake Waarabu baada ya kuanza kuwatoza kodi, kudhibiti biashara ya kwenda pwani na baadae kuzuia wasiuziwe nafaka. Mnywa Sele alisahau kuwa alifika hapo kwa nguvu ya Waarabu hao hao. Waarabu walipoona biashara na ustawi wao unatishiwa, mwaka 1860 walimpindua Mnywa Sele na badala yake wakamweka Mkasiwa kuwa mtemi wa Unyanyembe.

Mnywa Sele, kwanza alikimbilia Rubunga tawala ndogo kusini mwa Unyanyembe. Lakini Waarabu waliandaa jeshi na kwenda kumfukuza hapo nae akakimbilia Ukimbu ambako aliendesha vita vya msituni kwa miaka mitano akijaribu kurudi Unyanyembe bila mafanikio.

Katika jitihada za kujipatia mahitaji ya jeshi lake la ruga ruga, Mnywasele alianza kuvamia misafara ya kutoka pwani kwenda Unyanyembe.

Mwaka 1861 Speke alikutana na Mnywa Sele porini na la jeshi lake la ruga ruga. Speke alijaribu kutafuta suluhu kati ya Mnywa Sele na Waaraabu wa Unyanyembe bila mafanikio. Mnywa Sele aliuawa baada ya kushindwa na kukamatwa na msafara uliongozwa na Mwarabu Khamisi Bin Abdulla katika eneo kati ya Ugogo na Unyanyembe mwaka 1865.

Tukirudi Unyanyembe kwenyewe, watawala wa Unyanyembe hawakuridhishwa na kitendo cha Waarabu kumsaidia Mkasiwa kuwa mtemi wa Unyanyembe.

Wengi walimuona Mkasiwa kama pandikizi la Waarabu.

Mtemi Milambo ambaye alivutiwa na sera za Mnywa Sele za kuwatoza kodi Waarabu na kudhibiti biashara katika Unyamwezi, alimuona Mkasiwa kama kibaraka wa Waarabu.

Katika kipindi chote ambacho Mnywa Sele alipigana msituni, Milambo alimuunga mkono. Kwa hiyo uhasama kati ya Milambo na Waarabu na Unyanyembe ulichukua sura mpya.

Baada ya kumpindua Mnywa Sele na baadae kuuawa, Waarabu waliona kikwazo pekee katika kudhibiti biashara na siasa za Unyamwezi ni Milambo tu.

Milambo aliendelea kuwatoza kadi Waarabu na misafara yote iliyokuwa ikipitia Urambo kwenda Ujiji. Wagogo nao walikuwa na bugudha kubwa kwa misafara ya kutoka pwani kwenda Ujiji kupitia Unyanyembe kwa kudai hongo.

Kwa hiyo Waarabu walijikuta katika mazingira magumu kibiashara na kiusalama.

Mwaka 1871 Waarabu waliandaa jeshi kumkabili Milambo ili kufungua njia ya kwenda Ujiji.

Katika Kampeni hiyo Waarabu walisaidiwa na Mtemi Mkasiwa na mvumbuzi Henry M. Stanley ambaye msafara wake ulikuwa umezuiwa na Milambo kwenda Ujiji kupitia Urambo.

Jeshi la wapiganaji 2255 kati yao1500 wakiwa na bunduki na waliobaki wakiwa na silaha za asili.

Kwa mujibu wa kumbukumbu za Stanley, Milambo aliandaa rugaruga 1,000 akaunganisha na washirika wake Wangoni 1,500 kuwakabili Waarabu na washirika wao.

Baada ya kuombewa dua za kiislamu na tambiko za Kinyamwezi, Waarabu walianza mashambulizi kwa nyimbo za vita na tumbuizo za ngoma.

Milambo kwa ushujaa wake na utaalamu wa mbinu za kivita aliamuru majeshi yake yasipigane kwa nguvu badala yake wawe wanarudi nyuma kama vile wamezidiwa.

Kwa mbinu hiyo aliweza kuwavuta wavamizi hadi wakafika karibu na Ulyankulu kwa upande wa kaskazini.

Baada ya kuona majeshi yote ya wavamizi yameingia katika himaya yake, Milambo aliamuru majeshi yake yaanze kuishambulia.

Baada ya mapambano makali ya ana kwa ana jeshi la uvamizi lilivunjika na kusambaratika na kuanza kukimbia ovyo kurudi Unyanyembe bila ya mpangilio. Milambo aliwafuata na askari wengi wa wavamizi waliuawa. Alipofika Unyanyembe, Milambo aliharibu sehemu kubwa ya boma la Itetemia lakini hakuzingira sehemu alikojichimbia Mkasiwa wala sehemu alikokuweko Stanley.

Aidha Milambo hakuharibu ngome za Waarabu. Lakini ghafla Milambo aliisitisha mashambulizi ya Itetemia na kuamuru wanajeshi wake kurudi nyuma ingawa hakukuwa na upinzani mkali.

Hakuna maelezo yoyote kutoka kwa Milambo kwa nini alisitisha mashambulizi ya Itetemia.

Kuna mawazo kwamba huenda Milambo hakutaka kusababisha madhara yoyote kwa Stanley aliyekuwepo kwenye boma hilo na pia hakutaka kuingia kwenye mgogoro wa moja kwa moja na Sultani wa Unguja Zanzibar kwa kuwaangamiza Waarabu wa Unyanyembe.

Hata hivyo, wakati majeshi ya Milambo yanarudi nyuma mwarabu moja, Khamisi bin Abdulla aliamurisha wafuasi wake kushambulia kwa kudhani majeshi ya Milambo yalikuwa yameshindwa.

Alijidanganya. Mara moja majeshi ya Milambo ya yalizingira ngome ya Mwarabu huyo na kuuwa wafuasi wake wote pamoja na yeye mwenyewe na kuharibu kabisa ngome yake.

Kitendo cha kutomgusa Stanley ambaye alikuwa amekimbiwa na watu wake na kuwaacha Waarabu salama kinaonyesha jinsi Milambo alivyokuwa mwerevu. Hakutaka kuharibu uhusiano wake na jamii ya kimataifa.

Stanley alichukizwa sana na udhaifu walioonyesha Waarabu katika kampeni dhidi ya Milambo ambaye alimwita ‘’ Jambazi” na pia ‘’Bonaparte wa Afrika,” akimlinganisha na mfalme Napoleon Bonaparte wa Ufaransa.

Stanley alichukizwa na kitendo cha Waarabu kumwingiza kwenye mapambano na Milambo wakati wanajua hawana uwezo.

Stanley aliondoka Unyanyembe kwenda kusini ili kumkwepa Milambo. Alipita Ukonongo kisha akaelekea magharibi na baadaye kaskazini hadi Ujiji alikomkuta Dk. David Livingstone mwaka 1871.

Ushindi wa Milambo dhidi ya Waarabu wa Unyanyembe na washirika wao ulimfanya aonekane kama kiongozi asiye na mpinzani katika ukanda huu wa Afrika Mashariki.

Yeye mwenyewe alijiita ‘Sultan Mkuu wa Afrika’. Uhasama kati ya Milambo na Waarabu wa Unyanyembe uliendelea kwa kipindi chote cha uhai wa Milambo.

Jaribio jingine la Milambo la kuangamiza Unyanyembe na kuvunja kabisa nguvu za Waarabu lilishindwa. Septemba 1871 Milambo alishambulia Unyanyembe kwa lengo la kuwasambaratisha Waarabu.

Katika mapigano yaliyofanyika katika kijiji cha Mfuto karibu kabisa na Unyanyembe, Milambo alishindwa vibaya. Baadaye iligundulika kuwa, siku ile Milambo aliongoza mapigano akiwa amelewa.

Inawezekana tukio hili ndilo lililomfanya Milambo kuacha pombe kwani alimweleza mmisionari mmoja kuwa asingeweza kuendesha shughuli zote na kutawala watu wake vizuri kama angekuwa anakunywa pombe.

Kutokana na ushindi huo, Waarabu wa Unyanyembe waliamua sasa kumwangamiza Milambo. Waliandaa jeshi kubwa lililojumuisha Waarabu wa Unyanyembe, kikosi kilicholetwa na Waarabu wa Usangu, Mtemi Mulimanombe wa Ugunda, Mtemi Simba Kaung’ando wa Usawila na askari 300 walioletwa na Mwarabu wa Ujiji, Said Bin Majid.

Said bin Majid alitaka kutumia mwanya huo kulipiza kisasi kutokana na Milambo kumuua mtoto wake, Soud bin Majid na Mwarabu mashuhuri wa Unyanyembe Khamis bin Abdulla.

Khamis bid Abdulla ndiye aliyemuua Mnywa Sele (Msabila) ambaye Milambo alimuona ndiye mtemi halali wa Unyanyembe na siyo Mkasiwa.

Kuongozea nguvu mtemi Mkasiwa alipeleka wa rugaruga kwenye jeshi la Waarabu na yeye mwenyewe alikuwepo kwenye mapambano yaliyoongozwa na Said bin Salim, liwali wa Unyanyembe kama mwakilishi wa Sultan wa Zanzabir.

Dk. David Livingstone akiwa Ujiji alipata habari kuwa jeshi la Waarabu lilikuwa na watu 2,000. Katikati ya Mwaka 1872 Waarabu walishambulia Urambo.

Milambo alijua ukubwa wa jeshi la maadui lakini hakutishika sana.

Walipokuwa wanasogelea Urambo, Milambo alifanya shambulio kubwa na kuwashinda Waarabu na mara kikosi chote cha wavamizi kilisambaratika na kiongozi wao, Said bin Salim akakimbia kurudi Unyanyembe.

Wapiganaji baada ya kuachwa na kiongozi wao, kila mmoja alirudi kwao kwa njia aliyojua mwenyewe.

Kushindwa kwa Waarabu katika kampeni hii ambayo ilionekana kuandaliwa vizuri, Milambo alibaki bila tishio lolote katika udhibiti wake wa sehemu kubwa ya Unyamwezi.

Baadaye Milambo alipata washirika wakusaidiana naye. Wa kwanza ni Nyungu ya Mawe ambaye awali alikuwa anazunguka na jeshi lake katika misitu ya Ukimbu bila ya kuwa na makao maalumu.

Kisha alishambulia tawala ya Ukimbu ya Kiwele na kuishinda na kujifanya mtemi wa Kiwele na kuburi lake liko huko hadi leo.

Mwingine ni mtemi Mtinginya wa Usongo. Mtinginya na Nyungu ya Mawe waliwahi kupigana lakini baadaye walipatana na kwa pamoja wakawa washirika wa Milambo bila ya kuwa chini ya uongozi wa Milambo dhidi ya Unyanyembe na Waarabu wake.

Mshirika wa tatu ni Simba Kaung’ando wa Usawila. Huyu pamoja na Mtemi wa Ugunda walimsaidia Mkasiwa na Waarabu wake kumshambulia Milambo, lakini alibadilika na kufanya urafiki na Milambo.

Kwa kushirikiana na Watemi, Mtinginya, Nyungu ya Mawe na Simba Kaung’ando, Milambo alidhibiti njia zote za kwenda ziwa Tanganyika na Kongo na njia ya kaskazini kwenda Uganda.

Misafara yote iliyopita katika kipindi cha 1871 na 1879 ilifanywa hivyo kwa idhini yake na aliwatoza kodi. Kulikuwa na njia tatu, moja ilitoka pwani kupitia Ugogo na Unyamwezi* kaskazini kwenda Uganda.

Njia ya pili na maarufu ilipita Ugogo na Unyanyembe kwenda Ujiji na Kongo, na njia ya tatu ilipita Usagara, Usangu, Ukimbu hadi Karema katika Ziwa Tanganyika.

Milambo na washirika wake, Mtinginya na Nyungu ya Mawe walidhibiti njia ya kati ya Ugogo na Unyanyembe na kaskazini kwenda Uganda.

Kwa upande wa Kusini kwa kushirikiana na Nyungu ya Mawe na Simba Kaung’ando walidhibiti njia ya kupitia Ukimbu kwenda ziwa Tanganyika.

Wamisionari wawili, Tom Cadenhead na Frederick Carter walipojaribu kumkwepa Milambo kwa kupita njia ya kusini alipeleka jeshi lake kusini.

Kwanza alishambulia Ugunda iliyokuwa imesaidia Waarabu wa Unyanyembe na kisha akaingia Usawila bila ya mapigano kwa kuwa Simba Kaung’ando alifanya mapatano na Milambo.

Baadaye majeshi ya Milambo yakisaidiwa na majeshi ya Simba Kaung’ando yalimshambulia Mtemi Kasogela wa Upimbwe aliyekuwa amewapokea wamisionari hao wawili, Cadenhead na Carter.

Upimbwe iliangamizwa na wamisionari hao wawili wakauawa. Katika kampeni hiyo, Milambo alikuwa pamoja na majeshi yake. Kwa tukio hilo njia ya kupitia Usangu na Ukimbu ikafungwa.

Kwa udhibiti huo, Waarabu wa Unyanyembe hawakuwa na hiyari isipokuwa kupata kibali cha Milambo na kulipa kodi au ushuru wapate kufanya biashara katika eneo la Unyamwezi na hata kupitisha misafara kwenda Kongo.

Waarabu wa Unyanyembe hawakutaka tamaa katika harakati zao za kumwondoa Milambo wapate uhuru wa kufanya biashara ya watumwa na pembe za tembo.

Walimgeukia Sultan Barghash bin Said wa Zanzibar kumtaka apeleke jeshi kummaliza Milambo. Barghash alikubali kujiingiza kwenye mgogoro wa Waarabu wa Unyanyembe na Milambo siyo tu kwa sababu ya kuwasaidia lakini kwa sababu biashara ya pembe za tembo, ilianza kuyumba.

Soko la Zanzibar lilikuwa halipati pembe nyingi kama siku za nyuma.

Agosti 1873, jeshi la Bargash likiongozwa na Amir bin Sultan liliwasili Unyanyembe tayari kuungana na wenyeji wao kumkabili Milambo.

Kwa mshangao Waarabu wa Unyanyembe hawakupenda uteuzi wa Amir bin Sultan ambaye alishawahi kukaa Unyanyembe kabla ya kurejea Zanzibar na kusita kushirikiana naye.

Jeshi hilo ambalo liliundwa na Mabulushi kutoka Zanzibar na Waswahili kutoka Pwani baadaye liligawanyika.

Waswahili kutoka Pwani wakaendelea kumtii Amir bin Sultan na Mabulushi wakahamishia utii wao kwa Waarabu wawili wa Unyanyembe wenye ushawishi mkubwa Shaykh bin Nasibu na Abdulla bin Nasibu.

Ndugu hao wawili walihofu kunyang’anywa madaraka na ushawishi waliokuwa nao katika Unyanyembe na Amir bin Sultan.

Katika Mazingira ya mgawanyiko huo miongoni mwa Waarabu, uwezekano wa kumshambulia Milambo ukawa haupo.

Milambo alijua uwepo wa jeshi la Sultan Barghash hapo Unyanyembe lakini hakushambulia aliwasubiri wathubutu.

Sultan Barghash alimtuma Abdulla Mohammed kwenda Unyanyembe kuchunguza kwa nini Milambo hajashambuliwa. Mjumbe alitoa taarifa kwa Barghash kwamba hakukuwa na umoja miongoni mwa Waarabu kiasi kwamba kumshambulia Milambo isingewezekana.

Barghash kwa hasira akayaondoa majeshi yake kuyarudisha Zanzibar. Waarabu wa Unyanyembe walilalamika lakini Barghash akawajibu kuwa kama wanataka kuendeleza mgogoro na Milambo wanaweza kufanya hivyo kwa wakati wao.

Baadaye Barghasha alimwambia James Elton, mwakilishi wa Uingereza Zanzibar kuwa hana uwezo wa kufanya zaidi ya alivyofanya na mtazamo wake ni kuwaacha wakoloni wa Kiarabu waendeshe mapigano wao wenyewe.

Kisha akaongeza kuwa “hana mamlaka katika nchi hiyo (Unyamwezi)". Said bin Salim ambaye Wanyamwezi walimpa jina la Kissesa na ambaye Milambo alikuwa hampendi kabisa alipeleka ombi kwa Kabaka Mutesa I wa Buganda kumtaka alete jeshi kumwondoa Milambo.

Mutesa I alikubali na kuandaa jeshi la watu 9,000 kwenda Urambo.

Milambo mwenyewe alimueleza mmisionari, Dk. Ebenezar Southon aliyekuwa Urambo kuwa jeshi la Kabaka Mutesa I lilisitisha msafara na Kurudi Buganda baada ya kukosa maji ya kunywa kwa watu 9,000.

Kushidwa kwa kampeni ya Mutesa I dhidi ya Milambo kuliwaacha Waarabu wa Unyanyembe na njia moja tu ya kutafuta suluhu na Milambo.

Mwaka 1875 Said bin Salim alipeleka ujumbe kwa Milambo akitaka suluhu. Kilichozungumzwa na kukubalika hakikujulikana lakini matokeo yake ni kwa Milambo kuruhusu misafara ya Waarabu kupita katika himaya yake kwa kulipa ushuru.

Kampeni za kivita za Milambo katika sehemu kubwa ya Unyamwezi na kampeni za Nyungu ya Mawe katika eneo la Kusini na Kusini Mashariki ya Unyanyembe na harakati za Mtinginya Kasikazini Mashariki ya Unyanyembe zilifanya biashara ya pembe za ndovu katika soko la Zanzibar kudorora na Mkasiwa wa Waarabu wake hapo Unyanyembe kubaki kama wafungwa.

Mkasiwa hukuweza kutoka Unyanyembe kwa hofu ya wababe hao watatu. Kwa kulinda soko la Zanzibar na kwa kutotaka mapambano ya kijeshi, Sultan Barghash aliamua kumwekea vikwazo vya biashara Milambo hasa vifaa vya kijeshi kama bunduki, baruti, risasi na fataki.

Vikwazo hivyo vilimwathiri sana Milambo ingawa alivipata kwa njia ya uvamizi na kwa kununua kupitia watu wengine.

Milambo alianza kushindwa katika baadhi ya mapambano aliyoyafanya mwishoni mwa miaka ya 1870 na mwanzoni mwa miaka ya 1880.

Kwa mfano uvamizi aliofanya Milambo katika utawala wa Turu na Iramba ulishindwa na akalazimika kurudi nyuma.

Mwaka 1877 Barghash alieneza vikwazo vya silaha kwa machifu wengine zaidi ya Milambo katika eneo hili la Afrika Mashariki.

Milambo ameelezwa kuwa alikuwa mjanja, mwerevu na mwepesi wa kuchukua hatua wakati mwingine alikuwa mgumu kumuelewa.

Wangoni walipofika katika nchi ya Unyamwezi kuna wakati aliwatumia katika nchi ya rugaruga na wakati mwingine alitofautiana nao na kupigana.

Inasemekana kuwepo kwao katika jeshi lake kulimsaidia sana Milambo. Nyungu ya Mawe ambaye alikuwa mtawala aliyemtegemea kwanza Milambo, aliafiki harakati zake lakini baadaye alitamani Nyungu ya Mawe apunguzwe nguvu zake.

Ingawa baada ya mapatano na Waarabu mwaka 1875 Milambo alianza kuzungumza amani na kwamba vita sasa basi, lakini aliendelea kushambulia maeneo ya Ukongo hadi Ubende.

Milambo hakuvumilia uasi na utovu wa nidhamu. Hali hiyo ilipojitokeza ilizimwa kwa ukatili mkubwa. Viongozi wa tawala moja walipokataa kutii amri ya kuwataka wachangie gharama za jeshi yake, aliamuru wakamatwe na kuuawa.

Kijana mmoja aliyeibia msafara ambao Milambo alikuwa ametoa kibali, alikamatwa na alipofikishwa kwa Milambo, Milambo mwenyewe alimuua kijana huyo.

Milambo alikufa mwaka 1884 akiwa na umri unakadiriwa kuwa miaka 44. Mwaka huo huo alikufa Nyungu ya Mawe na Kabaka Mutesa I.

Maelezo ya kifo cha Milambo yana utata. Wazungu waliokuwepo katika eneo la Unyamwezi wakati wa kifo chake walisema alikufa kwa ugonjwa wa koo. Waliamini huenda ilikuwa ni saratani ya koo.

TAARIFA HII KWA MSAADA WA NASSORO WAZAMBI


MJUE MTEMI MILAMBO | Tesdo